Dhana ya tafsiri na tamthiliya kiswahili
Dhana ya tafsiri na tamthiliya kiswahili:
Mulokozi (1999:188), Anasema kuwa tamthiliya ni fani
ya fasihi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani
Wamitila,(2003:7) ameeleza kuwa, neno tamthiliya kwa
upana wake linatumiwa kujumuisha maneno drama na play kwa kiingera, kwahyo
tamthiliya ni utungo unaoandikwa kwa mtindo wa mazungumzo.
Tamthilia ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo
fulani katika matendo na mazungumzo (TUKI, 2004).
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa tamthilia ni utungo
au mchezo wa kuigiza matendo au mawazo fulani yaliyopo katika jamii, ambapo
huwa ni majibizano baina ya watu wawili au zaidi.
Catford (1965:20) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo
yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake
mawazo yaliyolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa).
Mwansoko, (2006) anafasili neno tafsiri ni zoezi la
kuhawilisha ujumbe kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.
Hivyo tunaweza kusema kuwa tafsiri ni kitendo cha
kufikisha ujumbe wa matini chanzi katika matini lengwa kwa kuzingatia muundo wa
lugha lengwa na maana ya lugha lengwa.
Pia tunaweza kusema kuwa tamthiliya tafsiri ni
tamthiliya iliyotafsiriwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine kwa
kuzingatia fani na maudhui ya kazi hiyo ya kifasihi.
Kwa mujibu wa Wafula, (1999).Anaeleza kuwa kuna aina
nne za tamthiliya zilizo tafsiriwa kama ifuatavyo, kwanza kuna tamthiliya
zilizo tafsiriwa kutoka lugha nyingine hadi kiingereza na kisha kutafsiriwa kwa
Kiswahili,mfano wa tamthiiya hizo ni pamoja na “MCHUUZI MUUNGWANA” yake
Moliere, nyingine ni “MFALME EDIPODE” yake Mbunda Msokile na ile ya “MKAGUZI
MKUU WA SERIKALI” yake Nikolai Gogol.
Pia kuna zile tamthilia zilizo andikwa kwa
kiingereza na wageni na kutafsiriwa kwa Kiswahili mfano wa tamthilia ilizo
tafsiriwa katika mfumo huu ni pamoja na tamthiliya zote za Shake
speare.Vilevile kuna tamthiliya zilizoandikwa asilia kwa kiingereza na Waafrika
kisha zikatafsiriwa kwa Kiswahili. “MASWAIBU YA NDUGU JERO” na “MZALENDO
KIMATHI” ni mifano ya tamthiliya. Kuna tamthilia zilizoandikwa katika lugha
nyingine za kiafrika na kutafsiriwa katika Kiswahili mfano wa tamthilia ni “
NITAOLEWA NIKIPENDA”.
Tamthiliya ya Kiswahili ni ile tamthiliya
inayojadili mambo mbalimbali yahusuyo utamaduni wa waswahili na iliyoandikwa
kwa lugha ya Kiswahili. Mfano; “KAPTULA LA MAKSI” yake Euphrase Kezilahabi na
“SAFARI YA CHINGA ”yake Shani Omary.
Zifuatazo ni athari chanja za tamthiliya tafsiri
katika tamthiliya ya kiswahili;
Taaluma ya
tafsiri imesaidia kuongezeka kwa machapisho mengi ya kazi za Tamthiliya, hii
imefanyika hasa mara baada ya kazi nyingi za tamthiliya kutafsiriwa kutoka
lugha nyingine nakutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili,mfano wa kazi zilizo
tafsiriwa na kuongeza idadi kubwa ya machapisho ni pamoja na “ADUI WA
UMMA”,”MKAGUZI WA SERIKALI” na “NITAOLEWA NIKIPENDA”. kazi zote hizi zimesaidia
katika kuendeleza ukuaji na kusambaa kwa tamthiliya.
Tafsiri inakuza lugha ya fasihi husika, kupitia
tafsiri msamiati mpya unaingia katika lugha husika tukijua kuwa lugha ndio
mhimili wa fasihi, kwa hiyo msamiati ukiimarika fasihi pia huimarika.‘Lugha
nyingi za kiafrika Kiswahili kikiwa miongoni mwao hazikuwa zimeendelea sana
kimaandishi hasa maandishi ya kufasili, kwa hiyo tafsiri za tamthilia zikilenga
kukuza maandishi ya lugha za Kiswahili. Na vilevile tamthilia ilitafsiri kwa
lengo la kuongeza machapisho ya fasihi ya kiswahili’’ (Ruhumbika 1978).
Tukianza na dhima ya kimaudhui, tumesema kwamba
tafsiri imeweza kuibua aina mpya ya maudhui. Hii ina maana kuwa kazi
inapotafsiriwa kutoka jamii lugha ambayo imepiga hatua kubwa kimaendeleo
kunakuwa na maudhui mapya ambayo yanaweza kuingizwa katika fasihi lengwa hivyo
kuweza kuamsha ari ya kimapinduzi. Kwa mfano inapotokea jamii yenye
ukandamizaji wa wanawake ila haina mwamko wa kupinga ukandamizaji huo wa
wanawake, jamii lengwa huwez kupata mwamko na kujifunza kwamba kukomeshwa kwa
ukandamizwaji wa wanawake ni jambo linalowezekana, mfano tamthiliya ya MTAWA
MWEUSI.
Kwa upande wa dhima za kifani, tunaona kwamba kazi
za tafsiri katika fasihi ya Kiswahili huweza kuibua mitindo mipya ya uandishi.
Jamii huweza kutofautiana na huweza pia kuwa na mitindo mbalimbali ya utunzi na
uandishi wa kifasihi. Hivyo, kazi ya fasihi inapotafsiriwa kutoka jamii moja
kwenda nyingine, jamii lengwa hunufaika na mitindo ya uandishi iliyopo katika
jamii chanzi. Katika tafsiri ulingalifu wa mitindo ni jambo la muhimu
sana.(Mwansoko na wenzake 2006). Mfano mtindo wa kishairi katika tamthiliya ya
MFALME EDIPODE.
Pia tafsiri huweza kusababisha kuingia kwa tanzu
mpya katika fasihi lengwa. Kama inavyobainishwa na wataalamu mbalimbali, tanzu
za fasihi hutofautiana kutoka jamii moja kwenda nyingine (Samwel 2012, Samwel
na wenzake 2013). Hivyo kazi fulani ya fasihi inapotafsiriwa kutoka katika
jamii moja kwenda nyingine ambayo haina utanzu husika, jamii lengwa hunufaika
kwa kuweza kupata aina mpya ya utanzu. Fasihi ya Kiswahili kwa mfano
imenufaishwa sana na utanzu wa tanzia ambao umeingizwa katika fasihi hiyo
kutokana na kazi za tafsiri za kifasihi kama vile Oedipus the king (Sophocles )
ambayo imetafsiriwa Kiswahili, MAFLME EDIPODE ((S. Mushi).
Katika dhima ya kutia shime na kuendeleza uandishi
wa kifasihi tunaona kuwa tafsiri imeweza kuwatia moyo waandishi na kuweza
kuandika zaidi. Mwandishi wa kifasihi anapoona kuwa kazi yake imetafsiriwa
katika lugha nyingine na kuoana hadhira pana, hummotisha kutunga zaidi. Aidha
kutokea mwandishi akaandika kazi yake ya fasihi na kukosa soko katika jamii
aliyoikusudia kutokana na sababu kama vile kukosekana kwa mwamko wa usomaji,
umaskini, ukosefu wa elimu na kadhalika. Katika hali kama hiyo, mwandishi
husika atanufaika na soko la nje kutokana na tafsiri na hivyo kutokata tama
kuandika zaidi. Mfano Ibrahimu hussen katika tamthiliya yake ya KINJEKETILE
iliyotafsiriwa kwa kiingereza.
Kupanua hadhira ya kazi ya fasihi. Kazi ya fasihi
inapotafsiriwa hupanua hadhira ya kazi ya kifasihi. Kazi hiyo hupata hadhira
pana zaidi na hivyo maudhui yake kuwafikia watu wengi zaidi kuliko kama
isingetafsiriwa katika lugha nyinginezo. Maudhui ya kazi ya fasihi huwalenga
watu hivyo, kama kazi husika itakuwa na hadhira finyu, mchango wa kazi hiyo
katika ukombozi wa jamii huwa mdogo pia. Mfano tamthiliya ya NITAOLEWA
NIKIPENDA ya Ngugi wa thiong'o.
Tafsiri huongeza msamiati wa lugha. Husemwa kwamba
jamii lugha hutofautiana katika mambo mbalimbali ikiwa pia ni utamaduni wa
kiwango cha maendeleo kilichofikiwa. Kazi ya fasihi ya jamii iliyopiga hatua
kubwa kimaendeleo inapotafsiriwa, huweza kusaidia jamii lugha yenye maendeleo
duni kuongeza msamiati. Msamiati wa lugha hutegemeana na kiwango cha maendeleo
kilichofikiwa. Lugha ya Kiswahili imenufaika sana na kazi hizi za tafsiri. Pia
hudaiwa kuwa lugha kama haitumiki haikui, hivyo kutafsiri kutaifanya lugha
itumike hivyo kukua, mfano MFALME EDIPODE, mapebari wa venis.
Tamthiliya tafsiri ni faida inayoongeza hazina ya
elimu katika kuzijua jumuiya mbalimbali, na kuzilinganisha na zetu ili
kukadiria maendeleo tunayotarajia kisiasa, kijamii na kielimu. Tafsiri kama
MABEPARI WAVENISI, JULIASI KAIZARI, MFALME EDIPODE, n.k. zinatekeleza jukumu la
kuijenga tamthiliya ya Kiswahili na kupanua viwango vyake kisanaa na
kitamaduni.Hivyo basi mbinu hii tafsiri imefanya fasihi ya Kiswahili kukua na
kuweza kuendelea kufanyiwa ulinganisho na fasihi nyingine za ulimwengu, mfano:
tamthiliya ya “AMEZIDI” ya Said A. Mohamed. Mfano wa kazi zilizotafsiriwa;
ALIYEONJA PEPO, NITAOLEWA NIKIPENDA yake ngugi wa thiong’o,” ADUI WA UMMA “na
“ORODHA”.Vilevile tafsiri imesaidia kuendeleza fasihi ya Kiswahili na utamaduni
wake katika jamii tofautitofauti kwa mfano, kuna kazi za fasihi ya Kiswahili
zikiwemo tamthiliya za Kiswahili zilizotafsiriwa ambazo ni pamoja na; “TUFANI”
ya Samweli S. Mushi, “SHETANI MSALABANI ”, “MTAWA MWEUSI”na “NITAOLEWA
NIKIPENDA” zake Ngugi wa Thiong’o.
MAREJELEO .
Catford J.C (1965). A linguistic translation theory
of : An easy in applied linguistics. London: Oxford press.
Method, S.(2015). Umahiri Katika Fasihi ya Kiswahi ,
Mwongozo Kwa Mwanafunzi na Mwalimu wa Fasihi Simulizi na Andishi. Meveli
Publishers (MVP).
Mwansoko H.J.M na wenzake (2006).Kitangulizi cha
Tafsiri : Nadharia na mbinu. Dar-es-salaam: TUKI.
Ruhumbika, G. (1978). Tafsiri za kigeni katika
ukuzaji wa fasihi ya Kiswahili . Makala.
Wafula, R.M (1999). Uhakiki wa tamtiliya , Historian
a maendleo yake . Nairobi Kenya: Jomo Kenyatta Foundation.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahil Sanifu. Dar es
salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Wamitila, K.W. (2003), Kichocheo cha fasihi simulizi
na andishi. English press: Nairobi.
Comments
Post a Comment