Jadili kwa mifano madhubuti majukumu ya fanani na mtambaji na kisha uoneshe mikakati na mbinu za utambaji wa hadithi.
UTANGULIZI,
Fanani ni mtendaji wa kazi za za sanaa za maonesho.
Vilevile fanani ni msani katika fasihi simulizi ambaye anasimulia hadithi,
methali, vitendawili, anacheza ngoma na anatumia lugha kueleza dhamira ya kazi
yake ya fasihi. Hivyo fanani anaweza kuwa msimulizi kama ilivyo katika ngano,
mwimbaji wa nyimbo au manju katika maghani, mtegaji katika vitendawili, mpiga
ngoma katika ngomezi au mlumbi katika ulumbi. Fanani aghalabu huwa msimulizi na
vilevile mshiriki katika fasihi simulizi (TATAKI 2014).
Mtambaji
ni mtu anayesimulia hadithi au ngano. Vilevile mtambaji ni mtu mwenye tabia ya
kujisifu au kwenda mwendo wa matao (TATAKI
2014).
Mikakati
ni mipango maalumu inayoandaliwa kwa ustadi mkubwa ili itumuke kama njia za
kufikia malengo Fulani (TATAKI
2014).
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa fanani ni mtendaji wa kazi za fasihi simulizi mbele
ya hadhira yaani kama vile maonesho, masimulizi ya hadithi na kuhusisha
matumizi ya lugha za ishara pamoja na miondoko ili kuweza kueleweka kwa hadhira
inayosikiliza na kutazama kazi hiyo ya fasihi ana kwa ana.
Yafuatayo ni majukumu ya fanani na
mtambaji katika utambaji wa hadithi
Hivyo
fanani na mtambaji katika kazi ya fasihi wana majukumu mbalimbali katika
utambaji wa hadithi kama ifuatavyo;
Fanani
na mtambaji hudumisha na kuendeleza lugha ya jamii yake, kwa mfano kadri fanani
na mtambaji wanavyofinyanga lugha ndivyo inavyopevuka na kukua. Fanani na
mtambaji hubuni mbinu mbalimbali ya lugha na kuipokeza. Kwa njia hii, lugha
hudumishwa na kuendelea kukua zaidi na zaidi (Wamitila, K. W, 2003)
Ingawa Fanani katika ngano si mmoja wapo wa wahusika wa hadithini, fanani huhusika katika
uwasilishaji wa hadithi. Fanani haiwakilishi tu hadithi bali huihusisha na kuifanya
kuwa sanaa tendwa pale anapoiwasilisha kwa hadhira hai (Balisidya, N, 1987).
Katika utegaji wa vitendawili, fanani (mtegaji)
huhusika kwa kutega vitendawili,
kupokea majibu na kuomba mji baada ya mteguaji (hadhira) kukosa jawabu.
Fanani hutunga tungo na huzisimulia au
kuziwasilisha kwa mfano, anayejigamba hutunga majigambo au vigugo na kuviigiza kwa
hadhira hai (Mulokozi, M.M. 1989).
Kupitia kwa uwasilishaji wake, fanani hufundisha
vijana mbinu za kuiendeleza fasihi simulizi kupitia kwa uwasilishaji wake.
Fanani
hutekeleza jukumu la kuelimisha hadhira.Fanani ana jukumu la kuonya, kuarifu,
kukashifu, kuelekeza, kufahamisha, kukosoa na
hata kuzindua hadhira yake
(Mulokozi, M.M. 1989).
Fanani huendeleza amali na utamaduni wa jamii yake
kwa kuupokeza kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kupitia kwa utambaji na hadhira, kwa mfano, fanani hudhihirisha mazoea ya mtambaji
na amali za kijamii zinazofumbatwa na ngano zenyewe kutoka kizazi kimoja hadi kingine (Wamitila, K. W, 2003)
Fanani na mtambaji hushirikisha hadhira
katika uwasilishaji wake, kwa vile fasihi simulizi ni tendi na ina hadhira hai,
ni jukumu la mwakilishaji ( fanani ) kuhakikisha kuwa hadhira yake inashiriki
kikamilifu (Wamitila, K. W, 2003)
Vilevile
mtambaji na fanani anapaswa kuwa na uwezo wa kuiwasilisha hadithi au ngano kwa
namna inayosisimua na kumchangamsha msikilizaji aua hadhira yake. Kufanikisha
jambo hili, fanani na mtambaji hawana budi kuwa wabunifu. Ubunifu huu
utamwezesha kuiwasilisha ngano ya mapokeo kwa njia inayoipa upya na upekee
Fulani kutoka kwa fanani na mtambaji mmoja hadi kwa mwanafasihi mwingine (Balisidya, N, 1987).
MIKAKATI NA MBINU ZA UTAMBAJI WA
HADITHI
Hadithi
huwasilishwa kwa hadhira kwa utendaji unaohusishwa na mikakati na mbinu maalumu.
Mbinu hizo ndizo misingi maalumu vitambulishi vikuu vya mtambaji wa hadithi.
Mbinu zenyewe ni kama zifuatazo;
Fomula ya
utangulizi/ufunguzi, hii ni sifa inayohuiana na uanzaji wa utambaji.
Hadithi za mapokeo katika jamii nyingi za kiafrika huwa na utangulizi au fomula
Fulani maalumu. Fomula au mtindo huu wa kuanza, mtambaji hurudiwa katika usimulizi
wote (Njogu, K. na Chimerah 1999). Jamii ya waswahili, kwa mfano, hutanguliza hadithi zao kwavitangulizi vifuatavyo;
Mtambaji;
Paukwa!
Hadhira;
Pakawa!
Mtambaji;
Paukwa!
Hadhira;
Pakawa!
Mtambaji;
Hapozamaniza kale………………..
Mtambaji;
Hadithi, hadithi!
Hadhira; Hadithi njoo!
Mtambaji;
Hadithi, hadithi!
Hadhira;
Hadithi njoo!
Mtambaji; Hapozamaniza kale………………..
Fomula za utangulizi hukekeleza
majukumu mengine madogo madogo kama yafuatayo:
i)
Huwa ni njia ya kuwavuta wasikilizaji pamoja, yaani kuivuta makini ya hadhira
inayomsikiliza.
ii)
Hutumika kumtambulisha mtambaji wa hadithi.
iii)
Huashiria na kuonyesha mwanzo wa adithi.
iv) Ni njia mojawapo ya kuweka mpaka wa wazi kati
ya ulimwengu halisi na ulimwenu wa hadithi.
Fomula ya Mwisho au fomula-kimalizio,
hii ni fomula inayopatikana katika sehemu ya mwisho wa hadithi za kimapokeo
katika jamii zilizo nyingi za kiafrika. Jamii nyingi humaliza hadithi zao kwa
kimalizio, “Hadithi ( ngano) yangu imekamilika hapo”, “……………………wakakaa raha
mustarehe” au “wakaishi raha mustarehe” (Njogu, K. na Chimerah 1999). Fomula kimalizio
hutekelaza majukumu yafuatayo:
i)
Huashiria mwisho au kumalizika kwa utambaji.
ii)
Huwa ni kama kitangulizi cha shughuli inayofuatia utambaji au utambaji mwingine
iwapo pana hadithi nyingine.
iii)
Iwapo pana mtambaji mwingine anayefuatia, basi fomula-kimalizio uwa kama
kiashirii cha kumwonyeshea kuwa anaweza akaanza.
iv)
Huwa ni njia ya kuwapumzisha wasikilizaji au kutuliza hadhira ambayo ilikuwa
imetulia na kuwa makini wakati wa usimulizi wa hadithi.
Virai-kaida, virai-kaida
aghalabu huwa ni vifungu vya maneno ambavyo hutanguliza hadithi au simulizi.
Virai hivi hupata jina lake kutokana na hali kuwa vinarudiwa na huwa kama kaida
Fulani. Mifano ni pamoja na “aliondokeo”, “hapo zamani za kale” na “aliondokea”
(Wamitila, K. W, 2003)
HITIMISHO; Hivyo mtambaji na fanani wana jukumu kubwa sana la
utambaji wa hadithi jukwaani kwa kuwa huwa na sifa zinazoubainisha na hadithi
zisomwazo vitabuni. Sifa hizi ni sehemu ambayo huipa utambaji utamu
usiopatikana tusomapo vitabu na majalida mengine. Hapa hadhira husikia sauti ya
mtambaji moja kwa moja. Isitoshe, utambaji na utendaji wake jukwaani una nafasi kubwa katika
kuuwasilisha ujumbe wake mbele ya hadhira. Kwa hiyo, utendaji-simulizi ni
utendaji unaotendeka pamoja na lugha. Utamabaji na utendaji huu hujumuisha sifa
mbalimbali ikiwemo na matumizi ya usemi halisi, urudiaji, tanakali sauti,
matumizi ya viashirii na viashiriaji, kuwepo kwa matendo ya uigaji, mtuo wa
kidrama, matumizi ya maleba, uimbaji wa sauti na mambo mengine mengi.
MAREJEO
Balisidya,
N. (1987) “ Tanzu na Fani za Fasihi
Simulizi” Katika Mulika Juzuu19. Nairobi University Press.
Mulokozi,
M.M. (1989) “ Tanzu za Fasihi Simulizi”
Katika Mulika Juzuu 21. Kurasa 1-24.
Njogu,
K. na Chimerah (1999) Ufundishaji wa
Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
TATAKI
(2014). Kammusi ya Kiswahili sanifu: Toleo la tatu. Dar es salaam: Oxford
University Press.
Wamitila,
K. W. (2003) Kichocheo cha Fasihi:
Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Books.
Comments
Post a Comment