Jadili wahusika katika riwaya yaMSAKOnaMAKUADI WA SOKO HURIA
CHUO KIKUU CHA STELLA MARIS
MTWARA
(chuo kikuu kishiriki cha mtakatifu Agustino)
KITIVO
CHA ELIMU
IDARA
YA KISWAHILI
KOZI : FASIHI LINGANISHI
MSIMBO : SW 324
MHADHIRI : MADAM KANWA
AINA
YA KAZI :
KAZI YA KIKUNDI
NAMBA
YA KUNDI: NAMBA
TANO
JINA
LA KIKUNDI : SHABAAN ROBERT
WAHUSIKA:
NA.
|
JINA LA MWANAFUNZI
|
JINSIA
|
NAMBA
YA USAJILI
|
SAHIHI
|
|
|
|
|
|
01.
|
ABDEREHEMAN MOHAMED R.
|
ME
|
STE/BAED/163047
|
|
02.
|
CHACHA ISACK
|
ME
|
STE/BAED/
163031
|
|
03
|
MAZOEA WADI
|
ME
|
STE/BAED/162854
|
|
04.
|
MITOTO BAKARI A.
|
ME
|
STE/BAED/162893
|
|
05.
|
MOLLEL
LIGHTNESS A.
|
KE
|
STE/BAED/162913
|
|
06.
|
MWAYA GOODLUCK J.
|
ME
|
STE/BAED/162912
|
|
07.
|
NANYENJE SALUM
|
ME
|
STE/BAED/162878
|
|
08.
|
RUKEHA ALESTER
|
KE
|
STE/BAED/162929
|
|
09.
|
SARAHAN, JUMA A.
|
ME
|
STE/BAED/162819
|
|
10.
|
TEMU JACKSON
|
ME
|
STE/BAED/162936
|
|
KAZI; Jadili wahusika katika riwaya yaMSAKOnaMAKUADI
WA SOKO HURIA
UTANGULIZI
Muhtasariwa riwaya
MSAKO
ni kitabu kilichotungwa na mwandishi maarufu wa Misri Naguib Mahfouz ambaye
alizaliwa mwaka 1911-2006 na kutafsiriwa na mwandishi Deogratius M. Simba mwaka
2004 kwa lugha ya Kiswahili na kupigwa chapa na Mkuki na Nyota.
Kama
jina la kitabu linavyojidhihirisha MSAKO, ni riwaya inayomuhusu Saber ambaye
alikuwa anamsaka baba yake Sayed el Reheimy ambaye hakuwai kumuona tangu
kuzaliwa kwake. Mama yake Saber, Basima
Osman anamuagiza Saber kwenda kumtafuta baba yake popote pale ulimwenguni.
Katika safari ya msako huo Saber anapitia maisha ya dhiki, chuki, faraja hadi
kupelekea kuhukumiwa kunyongwa baada ya kufanya mauaji ya Khalil Abdul Naga
ambaye ni mmiliki wa hoteli.
MAKUADI WA SOKO HURIA ni riwaya iliyoandikwa
na hayati Chachage S. Chachage mwaka 1999-2000 na kuchapishwa na E & D Publishers mwaka (2002). MAKUADI
WA SOKO HURIA ni riwaya inayochambua na kupembua mfumo wa kisiasa na kiuchumi
na mustakabali wa taifa la Tanzania. Ni riwaya ya kihistoria yenye ukweli
unaodhihirika leo. inatoa taswira ya mapambano ya watanzania katika kujipatia
uhuru na amani ya kweli. Ni mapambano dhidi ya ukoloni na baadae dhidi ya
baadhi ya watu walioteka nyara uhuru wa wengi na kushirikiana na wageni kupora
rasilimali ya nchi kwa kisingizio cha soko huria. Ni riwaya inayoweka bayana
uozo na udhalimu uliojificha katika mfumo wa soko huria ; tamaa, nguvu za
uchumi, ubinafsi, ukandamizaji, Dhuluma,Hujuma, Rushwa Utapeli, Siasa,UkalenaUsasa vimejadiliwa kwa kina katika
riwaya hii.
Wahusika Japhet Lupocho na Mwenerumango wanawakilisha
makuadi na wasaliti wengine ambao wameuponda uzalendo wao na kuwa vibaraka wa
wawekezaji au wabia.
Dhana ya wahusika
TUKI (1990:169), wamefasili
wahusika kuwa ni watu, miti au viumbe vinavyowakilisha watu katika kazi za
fasihi. Wahusika hutumiwa katika kazi za fasihi ili kuwakilisha hali halisi ya
maisha ya watu katika jamii inayohusika.
Madumulla
(2009) akiwarejelea Kasper na Wuckel (1982) anaeleza kuwa, mhusika ni picha
ambayo huchorwa na fasihi na ni kiini cha vitu vyote vipya, dhamira na mada
katika fasihi. Katika mhusika kuna uwili; mosi, kuna usawili wa kisanaa wa mtu
kwa upande mmoja; pili kuna sura ya mtu kwa upande mwingine. Ubunifu wa msanii
humuwezesha msanii kuwaumba au kuwasawili wahusika kinafsia, kiakili na
kimwili.
Msokile (1992), akimnukuu Penina Muhando wanasema kwamba wahusika
wanaweza kuumbwa kinafsia, kiakili na kimwili. Kutokana na ujenzi wa aina hii,
mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha mabadiliko
yake kilaanapokutana na mazingira tofauti. Ataonyesha mabadiliko katika
uhalisia wake kwa kuzingatianguvu zinazomzunguka kama vile za utamaduni, siasa,
uchumi na kadhalika.
kwa
ujumla, wahusika ni nyenzo kuu katika fasihi kwa sababuwahusika ndiyo dira ya
matukio na matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi inayohusika.Mtazamo
wa dhana ya wahusika hutofautiana kutegemea mkabala anaouchukua mhakiki
nanadharia ya fasihi inayohusika.Mhusika ni mtendaji katika kazi ya kifasihi na
huwa kielelezo cha viumbe wanaopatikanaulimwenguni, ingawa si lazima sifa zote
za mhusika zifungamane moja kwa moja na zawanadamu.
Aina za Wahusika
Wataalamu
mbalimbali wamegawa aina za wahusika kutokana na mitazamo yao. Miongoni mwa
wataalamu hao ni pamoja na hawa wafuatao; Ndungo na Mwai, (1991), Msokile
(1993) na Wamitila (2002) wameainisha aina tatu za wahusika ambazo ni; wahusika
wakuu, wahusika wasaidizi na wahusika wajenzi.
Wahusika Wakuuni wale wanaojitokeza kuanzia
mwanzo wa kitabu mpaka mwisho. Hata mara nyingine mhusika mkuu hutumiwa namsanii
kama kinywa chake. Yeye ndiye husema nakutenda msanii anayoyapendelea yaeleweke
katika jamii.
Wahusika Wadogo (Wasaidizi) ambao
wanaomzingira mhusika mkuu na wanaomsukuma aamue au asiamue jambo kinyume
chake. Wahusika hawa hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi. Wahusika
wadogo husaidia kuijenga dhamira fulani inayojadiliwa katika kazi ya fasihi.
Wahusika Wajenzi, niwahusika ambao kwa kiasi kikubwa
hutumika kwa lengo la kujenga au kukamilisha Maudhui ya kazi ya mwandishi. Pia
hutumika kushirikiana nawahusika wakuu na wahusika wasaidizi
Kwa
mujibu waNjogu na Chimerah (1999) wameainisha aina kuu nne za wahusika ambao
ni; Muhusika Mkwezwa, muhusika wa kisaikolojia, muhusika wa kimapinduzi na
mhusika jumui. Mhusika mkwezwanimuhusika
mwenye sifa za kiutendaji. Ni hodari na shujaa kama wahusika wa fasihi
simulizi.
Muhusika wa Kisaikolojia; Huyu ni muhusika anayekumbana
na matatizo mengi ya kijamii na anaibusha hisia za huruma kwa wasomaji.
Muhusika wa Kimapinduzi; huyu ni muhusika anayeelewa
historia, siasa, mazingira na hali ya kiuchumi ya jamii yake. Yuko radhi
kujitoa muhanga kubadilisha maisha ya wanyonge. Ana itikadi kali na msimamo
thabiti.
Muhusika Jumui; Ni muhusika wengi katika
mmoja.Hupatikana zaidi katika fasihi ya kidhanaishi. Muhusika huyo mmoja
anakuwa na sifa za wahusika wengi. Anatumiwa kuonesha fujo za maisha. Hivyo
anaitwa muhusika jumui. Mfano muhimu ni “mimi” na “sisi”.
Wahusika katika riwaya teule; MSAKO
na MAKUADI WA SOKO HURIA
Katika
kujadili suala la wahusika waliojitokeza katika riwaya hizo teule tunarejelea
nadharia ya uhalisia kama mwongozo wa mjadala huu.
Nadharia ya Uhalisia
Kwa
mujibu wa Wamitila (2000), nadharia ya uhalisia ni mojawapo ya matapo maarufu
katika ulimwengu wa fasihi na lenye athari kubwa sana. Dhana ya uhalisia
hutumiwa kwa maana mbili kuu. Maana hizo ni kuelezea tapo la kipindi maalum
katika fasihi na kuelezea aina ya mtazamo au tapo la kifasihi ambapo kazi za
fasihi zinachukuliwa kama zinavyohifadhi au kuakisi sifa za kimsingi
zinazohusishwa na uhalisi. Uchunguzi wa utanzu unaoambatana na uhalisi kwa kiasi
kikubwa hauwezi kuzungumzia riwaya bila ya kuyarejelea mawazo yanayohusisha
uhalisia. Wanauhalisia hufanya hivi ili kujifunga kwenye wahusika wa kawaida au
wanaoweza kupatikana katika jamii halisi. Kuyachunguza na kuyasimulia maisha
yao na tajriba zao na kusawiri kwa kuonesha mandhari na mazingira ya kawaida.
Tapo
hili limewekewa msingi na mwanafalsafa anaejulikanwa kama Hegel (1995) katika
kitabu chake Aesthetik (ujumi). Kuna
faida kubwa tatu zinazopatikana katika matumizi ya tapo hili. Kwanza, ni
kusisitiza uainishaji wa maisha ya jamii kupita wahusika kwa uaminifu mkubwa.
Pili, mtazamo huu unatia mkazo kwenye uwasilishaji kwa mambo ambayo yanaonekana
katika jamii inayohusika, na tatu hutoa nafasi ya kuyasawiri matukio, mandhari
na wahusika ambao huwenda wasiafikiane au wawafikiane na uhalisi wa jamii yake.
Kwa
kumrejelea Wamitila (2002:21), tunajadili baadhi ya wahusika waliojitokeza
katika riwayahizi kama ifuatavyo; Tukianza na riwaya ya MSAKO.
SABER, Huyu
ni mhusika mkuu ambaye habadiliki na hakui kisaoikolojia. Hii ni kutokana na
matendo yake na tabia zake kutobadilika. Mwandishi amemchora mhusika huyu Kama;
muuaji, mwizi, mhalifu, hana mapenzi ya kweli, ni malaya na mhuni. Mwandishi
hakuonyesha mabadiliko yoyote ya tabia ya mhusika huyu. Mwandishi amemchora
Saber kama mhusika mkuu ili kuonyesha kuwa katika jamii zetu kuna watu
wasiobadilika. Hafai kuigwa na jamii
SAYED SAYED EL-REHEIMY;
mhusika huyu amechorwa kama mhusika mjenzi. Huyu ndiye baba yake Saber.Yaani
amepewa sifa na uwezo uliopitiliza ukilinganisha na uhalisi wa maisha yake
yalivyo. Amechorwa kama mtu maarufu, mpenda starehe, tajiri na mwenye hadhi. Mfano
(uk9) mwandishi anaeleza sifa za muhusika huyu. Mhusika huyu amechorwa kama mtu
wa tabaka la juu kwani amekuwa mwakilishi wa tabaka la wenye nacho, pia, kama
mtu mbinafsi kulingna na tabia zake alizokuwa anafanya.
“Yeye ni mtu mwenye kipato kizuri
kabisa. Wakati huo alikuwa mwanafunzi bado, lakini hata wakati huo alikuwa na
uwezo wa kutosha na hadhi.”
Mhusika
huyu hafai kuigwa na jamii kutokana na tabia zake.
SHEHE,
Ni mhusika ambaye pia tumemfahamu kwa kusimuliwa (maizi), hivyo ni mhusika mjenzi
ambaye amewakilishwa dhahili, pia mhusika tunamtazama kama mtu anayewakilisha
tabaka la wanadini, kwani anawakilisha kundi la watu wanaoamini dini na watu
wanaoabudu. Mfano
“Shehe ambaye alikuwa ameketi huku amekunja
miguu akiwa katika tafakuri nzito, alisema, “tafuta na utapata.”(uk16)
Ni
kielelezo bora kwa jamii kutokana na kuwakilisha kundi la wanadini wenye imani
ya kweli. Hivyo anafaaa kuigwa katika jamii.
BWANA KHALIL ABDUL NAGA,
Huyu ni muhusika msaidizi ambaye huwa anakua kiakili na anabadilikabadilika na
ana sifa za uzuri na ubaya. Mhusika huyu tunamtazama kama mtu wa tabaka la juu
kwani anawakilisha tabaka la watu wenye kipato yaani matajiri na yeye ni
miongoni mwa matajiri wa jijini Cairo. Mhusika huyu ni mmiliki wa Hotel ya
Cairo, ni mme wa Karima, ni mzee kiumri, ameuawa na Saber. Kwa kiasi fulani
anafaa kuigwa na jamii kwa kuweza kuajiri watu wenye kipato cha chini ili
kuwainua kiuchumi. Kwa upande mwingine hafai kuigwa kwa tabia ya kutimia mali
zake kuwaoa mabinti wenye umri mdogo kama Karima.
ALY SERIAKOUS,
Huyuni mhusika msaidizi, ni kijana mwenye tabia nzuri, vilevile ni mhusika
ambaye amewakilisha tabaka la watu wenye kipato cha chini na wenye kuhangaika
na vibarua kila siku. Ni mchukuzi katika Hotel ya Cairo, ni kibarua wa Khalil,
alihusishwa na kifo cha Khalil, ni kijana mchangamfu na mchapakazi, pia
amesingiziwa kesi ya mauaji. Kwa kiasi kikubwa anafaa kuigwa katika jamii kwani
ni mhusika ambaye anapenda kuwasaidia watu.
ELHAM,
Ni mwanamke mchapa kazi na anafanya kazi katika ofisi za gazeti la sphinx na
ana sifa ya upole na mwenye huruma. Mchumba wa Saber, hamjui baba yake, ni mwanamke
msomi na anayejitambua, ana mapenzi ya kweli, ni mwanamke mwenye msimamo. pia
mhusika tunamtazama kama mfanyakazi anayependa kufanya kazi kwa bidii. Kutokana
na tabia ya mhusika huyu anafaa kuigwa katika jamii yetu ya leo.
KARIMA,
Ni mke wa Khalil, mwanamke asiye na huruma (mkatili) na ni msailiti, ambaye
mali zote za Khalil zipo chini yake. Tunaona kuwa ni miongoni mwa wauaji wa
bwana khalil na mwenye tamaa ya mali. Pia ni mhanga wa mila potofu, kwani
aliolewa na mwanaume asiyempenda kwa sababu ya umaskini na tamaa za pesa.Hivyo
ni mhusikaambaye tunamtazama kama mtu mbinafsi. Hafai kuigwa katika jamii kwani
ni kiwakilishi cha watu ambao hawana utu.
Pia
katika kitabu cha MAKUADI WA SOKO HURIA mwandishi amejadili wahusika na sifa
zao katika riwaya hii kama ifuatuatavyo;
Binti Wenga, huyu
ni mhusika mkuu katika riwaya hii, ni mhusika ambaye anawakilisha vyema nafasi
ya mwanamke aliye shupavu na mpenda maendeleo. Binti wenga siyo mtu mashuhuri
katika mambo ya siasa, Mama huyu hana ubinafsi bali anatumia uwezo wake katika
kutetea haki za nchi yake na wananchi kwa ujumla
“Alikuwa
ni mwanamke aliyeshuhudia ukombozi mpya, aliheshimiwa na wanawake wote na
kuhofiwa na wanume wa pale kijijini….(uk 111)”
Binti
wenga ni kielelezo cha wanamama wengi mahodari na majasiri katika jamii yetu,
hivyo anafaa kuigwa katika jamii.
Njovu Luhala;ni
mhusika msaidiziambaye amejadiliwa kwa kuwa na sifa ya kutetea tabaka la
wawekezaji ambao wananyonya wanyonge au wananchi kwa kuchukua maeneo na aridhi
zao bila malipo yoyote,Mbunge Luhala ni mwakilishi wa viongozi wa ngazi ya juu
wanaowakandamiza wananchi na kuwapora haki zao kwa kuwa na miradi kama ule wa
ufugaji wa kamba katika bonde la Rufiji, ambao haukuwa na budi kumilikiwa na
kuendeshwa na Wanarufiji wenyewe. Ni kielelezo cha viongozi wengine wengi
katika jamii ambao wanatumia madaraka yao kuwakandamiza wengine, kwani
anadiriki hata kumpa ujauzito binti mdogo akiwa katika majukumu yake ya kazi
huko bungeni, hivyo hafai kuigwa katika jamii yetu ya sasa.
Fidelis Mvumi Msakapanofu; ni
mhusika mkuu ambaye ni mwandishi wa habari pia ni msimulizi anayesimulia
hadithi ya riwaya nzima kwa kutumia nafsi yakwanza. Mhusika huyu ni mpambanaji
na mpenda haki ambaye anapambana kuweza kufichua mabaya yaliyo jificha juu ya
wananchi wa Rufiji ambao wana dhulumiwa ardhi na mabeparia wa kigeni kutokana
na mfumo hasi wa soko huria
unaowakandamiza wananchi na kuwanyima haki zao. Pia mhusika huyu anaenda kujuana
na ndugu au ukoo wake huko Rufiji baada ya kutengana nao kwa mda mrefu bila
kuonana. Kutokana na tabia njema ya kutetea haki ya wanyonge, anawakilisha
tabaka la watu wema katika jamii, hivyo anafaa kuigwa katika jamii.
Bwana Nyakilanzi;ni
mhusika msaidizi ambaye ni mwenyekiti katika kijiji cha Nyamisati ni kiongozi
bora anayependa maendeleo, kwani anawashilikisha wanakijiji wake katika kufanya
maamuzi na kupanga mipango na kuitekeleza kwa maslahi ya umma. Anakuwa mstari
wa mbele katika majukumu yote pale kijijini. Hana ubinafsi, na kwa misingi hii
huwa ni mtu wawatu mwenye kutetea wanyonge na haki zao katika jamii yake, hata
katika jamii yetu ya leo watu kama hawa wanopenda utu na Amani wapo. Mhusika
huyu ni kielelezo cha viongozi wapenda maendeleo na watetea haki za wanyonge
katika jamii, hivyo anafaa kuigwa katika jamii.
Alhaji Seif Said;ni
mhusika msaidizi ambaye anaonekana mwanzoni kuwa na msimamo wa kutaka kuisaidia
nchi yake kuondokana na unyonyajia na suala la ufisadi. Ni mwandishi wa habari
ambaye alifichua suala la uwepo wa mahindi huko Ruvuma, pia aliandika kuhusu
jinsi viongozi walivyo itelekeza meli ya India na bei ya ununuzi kuhusu zao la
korosho Mtwara na Lindi. hali iliyopelekea kupewa onyo kali na kuteuliwa kuwa
msajiri wa magazeti mwishoni mwa miaka ya themanini. Pia anakataa kusajili
gazeti la Fidelis ambaye alikuwa akiandika na kusuta juu ya mambo mabaya yanayofanywa
na baadhi ya viongozi wa serikali.
“Lazima litafungiwa. Haritarusiwa. Na mimi
nitahatarisha wadhifa wangu… (uk 18)”
Japhet Lupocho na Mwenerumango; wanawakilisha makuadi na wasaliti, ni waponda uzalendo wa
nchi yao na kuwa vibaraka wa wawekezaji, ni matajiri uchwara ambao wanakubali
kurubuniwa na mwekezaji mwingereza Paul Mooney kwamanufaa yao binafsi. Hawa ni
kielelezo cha matajiri wanaohujumu uchumi wa nchi hivyo kwa kiasi kikubwa
hawafai kuigwa katika jamii.
Paul Mooney na Balfour Beatty; wawekezaji mashuhuri nchini ambao wanatumia uwezo wao wa
kifedha kuteka mawazo ya Japhet Lupocho na Mwenerumango na hatimaye wanakuwa
wasemaji wa mwisho na kunyonya rasilimali za watanzania na kuwacha wananchi
wakiwa masikini, hivyo hawafai kuigwa na jamii.
Sifunina Mjuba;
ni wanaharakati wenye msimamo wa kimapinduzi. Kwa sababu ya kunusuru uuzwaji wa
Delta ya Rufiji wanatekwa na Kaboko, Mayasa na Willy. Ni wapenda maendeleo na
wanafaa kuigwa katika jamii. “…wale waandishi
wa habari walio nusuru taifa hili na janga la uuzwaji wa Delta ya Rufiji kwa
matapeli”
Oscar Mayowe; ni
mwandishi wa magazeti, ni msaliti na asiye na upendo wa dhati. anampa mimba
binti waziri, anakubali kuvunja uhusiano na mkewe ili amuoe binti waziri.
Kutokana na tabia yake ya usaliti hafai kuigwa katika jamii. “Ndoa mahususi ya kiislamu inatarajiwa
kufanyika mwezi wa tatu”.
HITIMISHO
Pamoja
na kwamba waandishi wa riwaya hizi wana asili tofauti lakini bado kazi zao zina
mfanano mkubwa kuliko kutofautianaRiwaya hizi za MSAKO na MAKUADI WA SOKO HURIA
ni riwaya zinazosawili mazingira halisi ya jamii za nchi zinazoendelea barani
Afrika. Kwa mfano waandishi wa vitabuu vyote wamewatumia waandishi wa habari
ikiwa kama ni njia ya kutatua matatizo yanayoikabili jamii husika; mwandishi
amemtumia mhusika Elham na Tantawi katika kitabu cha MSAKO kutoa msaada wa
kumtafuta baba wa Saber, lakini pia mwandishi amewatumia wahusika kama vile
Fidelis, Sifuni, Mjuba, na wengine kuyasemea yale maovu yote yaliyotokea katika
jamii ya watanzania.
Katika
suala la kutofautiana kwa wahusika wa riwaya hizi mbili tunaona kwamba, kwa
kiasi fulani riwaya hizi zinatofautiana, tukianza na waandishi wenyewe
tunagundua kuwa Naguib
Mahfouz
ni mzaliwa wa Misri na kwa upande wa Chachage S. Chachage ni mzaliwa wa Tanzania hivyo wanatoka
katika tamaduni tofauti. Lakini hata pia kupitia wahusika tunagundua kwamba
riwaya ya MAKUADI WA SOKO HURIA imejikita katika kufanya mapinduzi ya
watanzania kujikomboa na udhalimu wa kipebari, wakati riwaya ya MSAKO imejikita
katika msako wa Saber kama jina la kitabu linavyodokeza.
Kupitia
dhana ya wahusika waandishi wameweza kuwachora wahusika katika namna mbili,
wale wafaao kuigwa na wale wasiofaa kuigwa kutokana na matendo na tabia zao. Hivyo
kupitia wahusika, jamii inaweza kubadilika kimtazamo chanya au hasi kwa kuwa
kazi ya fasihi lazima iache athari katika jamii husika.
MAREJEO
Chachage,
Chachage Seithy L. (2002). Makuadi wa Soko Huria. Dar es Salaam: E & D
Publishers Limited
Madumulla, J. S (2009). Riwaya
ya Kiswahili. Dar-es-salaam: Mture Educational Publishers
Mahfouz,
N (2004). Msako. Dar-es-salaam: Mkuki na Nyota Publisher
Msokile,
M. (1992). Kunga za Fasihi na Lugha. Dar-es-salaam: Educational Publishers and Distributors Ltd
Njogu,
K. na Chimerah, R. (1999). Ufundishaji wa Fasihi Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation Ltd
Ndugo,
C. M na Mwai W. (1991). Historical and Modern Development of Kiswahili. Nairobi University Press. Nairobi
TUKI,
(1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Taasisi ya uchunguzi Tanzania. Dar-es-salaam: Chuo Kikuu
Wamitila,
K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi Msingi na Vipengele Vyake. Phoenix Publisher
Ltd
Comments
Post a Comment