Jadili dhana ya neno huku ukitathimini utata uliopo katika kutoa tafsiri hizo ukirejelea mitazamo ya wataalam mbalimbali wa isimu.




UTANGULIZI
Habwe na Karanja (2004) wamefafanua neno kama kipashio cha kiisimu chenye maana kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.
Katamba (1994) anasema kuwa neno ni kipashio kidogo chenye maana katika lugha ambacho kina dhima kisarufi . Neno linaweza kusimama peke yake na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine.
Mfano neno ‘childish (utoto) linaweza kutenganishwa na kubaki ‘child` (mtoto) na neno hili linaweza likatumika kiupwekeupweke kwa sababu ni neno linalojitegemea lakini hatuwezi kutenganisha kipande ‘-ish` (kama ilivyo katika Kiswahili) kikasimama peke yake na kuleta maana.
Massamba na wenzake (2003) wanabainisha kuwa neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo-sauti (yaani kuchunguza sauti zinazounda umbo zima) kiothografia yaani herufi na kisarufi kile kinachowakilisha umbo husika.
Chomi (2003) anaeleza kuwa neno ni mzizi tu au ni muundo wa mzizi pamoja na kiambishi kimoja au zaidi.
Delahunty&Garvey (2010) wanasema kuwa neno ni vipashio vigumu vinavyoundwa na vipashio kadhaa vya msingi vinavyoitwa mofimu.
Ni kweli kwa dhana ya neno  ni tata katika kuifasili utata huu unatokana na vigezo mbalimbali vya kisarufi ambavyo wahisimu huvitumia kama muongozo wa kufasili dhana hii kama ifuatavyo;                                                                                                                                                                                             kigezo cha kileksika
Kigezo hiki hueleza kuwa neno ni kipashio cha kileksia chenye udhahania ambacho huweza kudhihirika kimaana na kikazi kipashio hiki huweza kuwakilishwa kimaandishi au kimatamshi kwa mfano; Mdee (2010) akimrejelea Crystal  (1980) anaeleza kuwa leksimu ni kipashio dhahania kinachowakilisha maumbo kadhaa yanayotokana nacho.
            Mfano
              Refu              -ndefu                                                                                                                                                                                                              
  Mrefu            -kirefu
Utata wa kigezo hiki
Hakiweki bayana juu ya maumbo yatokanayo na leksimu moja kuwa ni maneno tofauti au neno moja. Kuna maneno yenye umbo moja lakini huwa na maana tofauti, Je maneno hayo yatakuwa ni neno moja au ni maneno tofauti?
Kwa mfano     Paa    -sehemu ya juu ya nyumba   –mnyama, enda juu au angani                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                            Panga   -kifaa cha kukatia kuni      -kitendo cha kuweka vitu sawa
Kigezo cha kiothografia
Kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni maandishi yanayoacha nafasi mwishoni. Neno hudhihirika katika maandishi  tu na lisiwe na nafasi  katikati. kwa mfano  Rubanza (1996) anaeleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati.
Mfano katika sentesi; Baba analima shambani. Sentensi hii ina maneno matatu yaliyopigiwa mstari. Pia maneno kama; mwana-chama, paka-shume huchukuliwa kama maneno mawili tofauti Katika lugha ya kiingereza maneno kama ‘blackboard’ na 'cannot” yanachukuliwa kama neno moja
Utata wa kigezo hiki
Huchukulia maneno ambatani kuwa ni maneno mawili tofauti kwa sababu huandikwa kwa kuacha au kutenga nafasi katikati. Dai hili si kweli kwa sababu maneno ambatano hurejea dhana moja hivyo hupaswa kuchukuliwa kama neno moja. Mfano Bata mzinga.
Pia kigezo hiki kimejikita katika lugha ya maandishi tu na kutupilia mbali lugha ya mazungumzo, kwani tunapoongeza  nafasi tupu huwa hazionekani. Hivyo  tunajiuliza maswali. Je neno ni lile linaloandikwa tu?

Kigezo cha kifonolojia
Kigezo hiki huchukulia neno kama ni kipande cha lugha kinachotokana na kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi. Kutokana na kigezo hiki kuna vigezo fulani vilivyowekwa ambavyo hutofautiana kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Rubanza (1996) anaeleza kuwa zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Hasa zile lugha zenye kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Sehemu iyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno au silabi ya pili kutoka mwisho. Kwa mfano katika lugha ya kiingereza                                                      
I didn’t  take the test yesterday”.
Sentensi hii ina maneno matatu yaliokolezwa wino, kwa sababu mkazo huwekwa kwenye maneno yenye kubeba maana.
Utaratibu huu si mara zote kwa kuwa kuna wakati hata yale maneno yasiobeba maana (grammatical words) hubeba mkazo kwa sababu ya msisitizo wa neno au maneno katika sentensi.                                                                      
Mfano: katika sentensi ileile I didn’t take the test yesterday” ikiwa mzungumzaji ataweka  mkazo katika “I”atakua akionyesha msisitizo siyo yeye,”didn’t” hakufanya,na the”  akimaanisha hakufanya jaribio hilo (lililokusudiwa na muulizaji)
Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho.             
Mfano: anacheza, analima.
Kigezo hiki kinasaulia kutofautisha maneno kwa kutumia mkazo,hususani katika lugha ambazo mkazo hua na uamilifu wa kubadili kategoria ya neno.Mfano katika lugha ya kingereza; ‘respect (nomino) respect (kitenzi).
Utata wa kigezo hiki
Kinashindwa kuweka bayana neno hasa ni lipi,kwani tunaona kuna baadhi ya vipande-Lugha visivyobeba maana ya msingi kama vile viunganishi na vihusishi katika lugha ya Kiswahili ambavyo haviwekewi mkazo.Swali ni kwamba,je vipande lugha hivyo ni maneno au si maneno?
Kigezo cha maana
Katika kigezo hiki wanaisimu husisitiza maana katika kufasili dhana hii kwa kudai kuwa  neno lazima liwe na maana.Kwa mfano Mdee (2010) anaeleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana. Neno lazima liwe  na maana.
                Mfano;
Baba –mzazi wa kiume
Mama-mzazi wa kike
Hivyo kwa kutumia kigezo hiki, neno hutambuliwa kuwa ni kipashio cha kiisimu chenye maana.
Utata wa kigezo hiki.
Kigezo hiki hakibainishi kuwa ni maneno yapi hulengwa  hasa kwani kwa kiasi kikubwa kinaegemea sana katika maana ya kileksika na kusahau mambo yenye maana kisarufi kama viunganishi na vihusishi.
Hakiweki wazi juu ya maneno yenye maana ya mficho.
Kwa mfano;Amepata jiko -Ameoa
                 Mkono wa birika -Mchoyo
Pia maneno yenye maana zaidi ya moja. Kama vile; mbuzi, paa na kata
Maneno haya yakisimama peke yake huwezi kupata maana moja hivyo lazima yawe katika mahusiano na mengine katika sentensi ndipo upate maana.
Kigezo cha neno kama kipashio huru kisichogawanyika
Bloomfield (1993),anasema neno ni umbo dogo kabisa  lililo huru. Fasili hii ina mambo makuu mawili, kwanza neno liwe “umbo dogo” pili “umbo huru”. Hapa umbo dogo  humaanisha umbo ambalo haliwezi kugawanyika bila kubadilisha maana yake.
Kwa mfano; neno Paka-huwezi kuligawa katika “pa” na “ka” bila kupoteza maana yake. Hivyo umbo dogo ni lile ambalo linashikilia maana.
Kwa upande wa neno kuwa huru ina maana kwamba neno hilo lazima litamkwe peke yake bila kutegemea au kuhambisha kwenye  neno lingine.
Mfano; njoo, lete na jua.
Utata wa kigezo hiki
Neno linalopewa uzito ni lile lililo katika lugha ya mazungumzo pekee. Katika lugha ya maandishi tunaweza kuwa na vipande vidogo vya maneno lakini ambavyo vikiwa huru hatuwezi kusema  vina maana kwa kuwa  huwa havirejelei kitu au hali yeyote ile.
Mfano katika lugha ya Kiswahili vipande “kwa”, “cha” na “tu” havina maana vikiwa peke yake bali hubeba maana vikiambatana na maneno mengine kama vile “kiatu cha baba”.
Kigezo cha kisemantiki na kiprogmatiki
Katamba (1993) anasema ili neno litambulike lazima liwe katika muktadha wa matumizi. Neno moja  linaweza kuwa na dhima mbalimbali  na dhima hugundulika inapokua ndani ya muktadha wa matumizi kwenye sentensi. Anatoa mfano wa neno la kiingereza “cut” kwamba likiwa kiupweke upweke huwezi kutambua linarejelea nini,pamoja na kwamba katika lugha ya kiingereza ni kitenzi “kata” lakini kuna wakati  linaweza kutumika kurejelea nomino .
Mfano; “I need my cut” na “I have cut my finger” katika mifano hii neno “cut” katika sentensi ya kwanza rejelea nomino yaani “nahitaji stahiki yangu”. Katika sentensi inayofuata linarejelea kitenzi yaani nimekata kidole changu. Neno la Kiswahili  “chungwa” huwezi kutambua linarejelea nini. Hii ina maana kuwa neno hili linaweza kutumika kama nomino au kitenzi.
Kigezo hiki pia huenda mbali kwa kufafanua kuwa pia maneno kama ; na, tu, si  katika Kiswahili na maneno, and, an, the, on katika kiingereza nayo hayawezi  hutambulika yanarejelea nini. Lazima yawe katika muktadha wa matumizi ndio tunaweza kusema ni aina gani za maneno au kutambua maana zake.



Utata wa kigezo hiki
Ni kwamba si lazima maneno yote yawe katika muktadha wa matumizi ndipo tuweze kubaini maana zake, kwani kuna baadhi ya maneno huweza kutambulika kuwa yana maana gani hata yasipokua katika muktadha wa matumizi katika sentensi. 
Kwa mfano nomino za mahali kama vile; Dodoma, Mwanza na Morogoro na majina ya watu kama vile; Amina, Omari, Fatuma  na Ali. Swali la kujiuliza kuwa aina hizi za nomino na nyingine nyingi ambazo ni kama hizi  je si maneno? Tunaona pia kigezo hiki hakijajitosheleza katika kutupatia maana ya “neno” itakayokidhi mahitaji ya taaluma zote
                                                                   HITIMISHO                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                          Pamoja na vigezo mbalimbali vilivotumika kufasili dhana ya neno kuonekana ndicho kiini cha ugumu wa fasili ya neno, tofauti ya lugha nazo huchangia kufanya fasili ya neno kuwa ngumu.                                                                                                                                                                
Hii ni kwa sababu  tabia ya lugha hutofautiana kwani  neno linaweza kuwa neno katika lugha fulani lakini lisiwe neno katika lugha nyingine.
Pia mitazamo tofauti tofauti ya wataalamu nayo ni sababu nyingine ya ugumu huo. Hivyo ni muhimu kujifunza mofolojia kwa kuzingatia vigezo na mawazo ya wataalamu tofautitofauti katika kuielewa dhana ya neno.
Katika taaluma ya mofolojia neno linaweza kutumika utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa maneno. Kimsingi  taaluma hii hushughulikia muundo wa ndani wa neno ambao hujengwa na maumbo yaitwayo mofimu ambayo hufanyiwa tafiti katika taaluma hii. Dhana hii husisitiza kuwa kitovu cha uchunguzi wa kimofolojia ni neno. Hivyo  basi dhana ya neno huweza kuwa ni kipashio cha kiisimu chenye maana kinaundwa na mofimu moja au zaidi       
MAREJELEO
Habwe, J. na Karanja, P. (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili: Phonix Publishers Ltd. Nairobi.
Katamba, F (1994) English Words Routledge: London.
Massamba D.P.B., Kihore, Y & Hokororo, L (2003) Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA) Sekondari na Vyuo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Chomi, E.W. (2013) Kitangulizi cha  Mofolojia ya Kiswahili Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Delahunty, G.P& Garvey, J.J. (2010). The English Language from Sound to Sense. Collins Colorado.

Comments

Popular posts from this blog

International Law

KATIBA YA KIKUNDI