Kituo, kiishio au kibwagizo

 Mashairi ya kisasa ni mashairi yasiyozingatia kanuni za kimapokeo, yaani, hayazingatii kanuni za muwala/urari (ulinganifu) wa mizani, vina, idadi ya mistari katika kila ubeti na kituo katika shairi. Mashairi haya pia huitwa mashairi huru / mashairi ghuni / mashairi ya kisasa / masivina /mapingiti

Muhimu ni kwamba wanausasa wamevunja kaida, kanuni, sheria na mitindo ya uandishi wa ushairi wa kimapokeo. Hii haimaanishi kwamba sheria zote zimetupiliwa mbali, bali mtindo mpya unaojitokeza katika uandishi wa ushairi unafinyanga mbinu za awali na mpya na kutupa taswira mpya kabisa ya ushairi. Kwa mfano mshairi aweza kutiririsha vina mahala popote katika ushairi, Idadi yoyote ya mizani inaweza kutumiwa katika tungo tofauti. Kumejitokeza na mashairi yenye michanganyiko mbalimbali ya maumbo, takriri, mizani maadamu ufinyanzi tofauti. Mbali na haya utunzi wa ushairi wa kisasa unaegemezwa sana kwenyematumizi ya lugha kama nyenzo muhimu ya kusanifu ushairi.

Ndipo sasa Mulokozi na Kahigi (1979: 25) ambao ni wafuasi wa ushairi wa kisasa wanapendekeza fasili ifuatayo:  Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha, au sitiara, au ishara, katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbo, ili kuelekeza wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu, kwa njia inayogusa moyo.

Mawazo haya yanatokana na fasili za washairi wa kisasa kuhusiana na swala la je ushairi wa Kiswahili ni upi. Uteknolojia huu wa kimchanganyiko ndio namna mwafaka kwao wa kuonyesha usanii, uhodari, ustadi na ubingwa wa kiutunzi. 

Ufuatao ni usasa unaojitokeza katika mashairi ya kisasa hasa katika muundo wake

Idadi ya mistari/ mishororo katika kila ubeti,

Wanausasa kwa upande wao wakiongozwa na Euphrase Kezilahabi wanasema kwamba shairi si lazima liwe na mistari mine katika kila ubeti ndiyo liwe shairi kama wasemavyo wanamapokeo bali Shairi linaweza kuwa na idadi yoyote ile ya mistari kutegemeana na nia na utaalamu wa mshairi katika kutunga mashairi yake. Kwa mfano, katika shairi la "Mafuriko"

anasema:

              "Nitaandika wimbo juu ya mbawa za inzi

              Utoe muziki arukapo wa usikie walio wengi

              Ushairi wa jalalani utaimbwa

              Juu ya vidonda vya wakulima

              Na usaha ulio jasho lao

              Nitaandika juu ya mbawa za wadudu

              wote warukao".

             "Juu ya mistari ya pundamilia

             na masikio makubwa ya tembo,

             Juu ya kuta vyooni, maofisini, madarasani

             Juu ya paa za nyumba na kuta za Ikulu!

             Na juu ya khanga na tisheti

             Nitaandika wimbo huu".

Katika shairi hili Euphrase Kezilahabi ametumia mistari saba katika ubeti wa kwanza

na mistari sita katika ubeti wa pili.

Idadi ya vipande katika kila ubeti, mashairi ya kisasa mengi huwa idadi kamili ya vipande yaweza kuwa kimoja, au hata vitatu ambapo huwa ni kinyume na yale mashairi ya kimapokeo ambayo huwa na vipande viwili.kwa mfano katika shairi la "mama angu" la Said Ahmed Mohammed (2002: 24-27) ni moja ya shairi la kisasa ambalo lina kipande kimoja. Mfano

"Una siri mama’ngu!

Umezongwa kitandawili!

Yaendaje maisha yako?

Hata mimi sikuelewi".

(uk. 25)

 Vipande vitatu  Mfano katika shairi la "Moyo" lililopo katika Wamitila (2005) kwenye ubeti ufuatao:-

"Moyo waniambia ota, kuwa mwizi usiote, siwezi kaini,

Moyo unaniambia kata, milija yote ikate, mizizini,

Moyo waniambia teta, penye dhuluma patete, andikoni,

Moyo waniambia woga, ndio mwanzo wa maafa"

Katika beti huu, kipande cha kwanza huitwa ukwapi, kipande cha pili huitwa utao na kipande cha tatu huitwa mwandamizi.

       Kituo, kiishio au kibwagizo,

Kibwagizo ni yale maneno ambayo mtunzi wa ushairi anayotumia kama kituo katika

ushairi wake.wana usasa hawandiki beti zao za ushairi wao kwa kuziwekea kibwagizo

kinachofanana, bali kibwagizo kinakuwa ni tofauti katika kila ubeti. Isitoshe; kila

kibwagizo ni kipande kimoja tu cha msitari si vipande viwili kwa msitari kama ilivyo

kuwa wanamapokeo.Kwa mfano Euphrase Kezilahabi katika shairi la "Dhifa" anaandika:

                     "Ni chakula cha mchana,

                       Walanchi wameshafika,

                      Wazungu, Wahindi, Waarabu

                      Washateka sehemu zao

                      Chakula ki mezani

                           Nidhifa".

                     "Mawaziri wenye kula,

                      Wabunge wapewa magari,

                      Waandishi waliosajiliwa,

                      Watangazaji wenye yale yale,

                      Wakereketwa wasokereka,

                      Kimya wamekaa", (uk. 27).

Hizi ni beti mbili za shairi moja lakini zinatofautiana katika kibwagizo chake. Kila

ubeti una kibwagizo chake ambacho ni msitari mmoja tu ama nusu msitari.

Ulali wa vina na mizani katika kila ubeti,

Euphrase Kezilahabi kwa upande wake haandiki ushairi kwa kufuata urari wa vina

na mizani. Anaandika hivi kwa sababu anaeleza kwamba, shairi si lazima liandikwe

kwa kuzingatia urari wa vina na mizani ndiyo liitwe shairi. Mawazo haya yanaungwa

mkono na Mulokozi (1975) pale anaposema kwamba, "ushairi wa Kiswahili

hautambuliki kwa vina na mizani bali utamaduni na lugha yake". Katika kuthibitisha

mawazo haya Euphrase Kezilahabi ametunga mashairi ambayo hayafuati urari na

vina na mizani. Kwa mfano: Katika shairi la "Mafuriko" anasema:

                     "Mti mkongwe umelalia upande

                        Wa nyumba zetu hafifu

                        Upepo mkali uvumapo hatulali

                        Kila kukicha twatazama mizizi yake

                         Na mkao wake, na kuta hafifu za nyumba

                         Lazima ukatwe kuanzia matawi hadi shina

                          Mafuriko ya mwaka huu yaashiria

                         Tutabaki kuwasimulia wajukuu

                          Mwaka ule wa mafuriko

                          Miti mingi mikongwe iliaanguka," (uk.4).

Shairi hili halina urari wa vina wala mizani na wanusasa wanaliona hili kuwa ni

shairi na si vinginevyo.

Hitimisho, pamoja na usasa katika mashairi ya kisasa yamekusudiwa kuburudisha jamii, kuhamasisha jamii, kukuza sanaa na ukwasi wa lugha, kuliwaza, kuelimisha, kuonya, kutahadharisha, kusifia mtu au kitu na kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 Marejeleo

Kahigi, Kulikoyela & Mugyabuso Mulokozi. (1973). Mashairi ya Kisasa. Dar es Salaam:

Tanzania Publishing House.

Kahigi, Kulikoyela & Mugyabuso Mulokozi. (1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es

Salaam: Tanzania Publishing House.

Mlokozi,M.M na Kahigi,K.K (1979), kunga za ushairi na diwani yetu,Tanzania publishing house; Dar es salaam

Comments

Popular posts from this blog

International Law

KATIBA YA KIKUNDI