Utendi

 

   UTANGULIZI

wamitila (2003) Uk 333 ," Utendi; Ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu mateso ya mashujaa au shujaa".

Mulokozi (1996) uk 85, " Utendi ; Ni utungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa kwenye jamii au taifa.

Utendi simulizi:  Ni utungo simulizi wenye mtindo wa kifomula unaohusu mambo ya ajabu ya watu wasio wa kawaida (mashujaa) na masimulizi hayo husimuliwa kwa njia ya mdomo. Ili hali, Utendi andishi; Ni ushairi wenye kusimulia matendo ya shujaa au mashujaa kwa njia ya maandishi.

Hivyo basi, Utendi ni maktaba ya jadi ya historia ya jamii fulani ambayo kupitia tendi mbalimbali jamii inatambua historia yake, mashujaa wao pamoja na mila na desturi zao.  Na zifuatazo ni hoja zinazotofautisha kati ya utendi simulizi na utendi andishi;

 Utendaji_uwasilishaji; Ni kitendo cha kuelezea mtu ama kitu namna kilivyo kwa kuonyesha sifa zake .  Hivyo basi utendaji_uwasilishaji ni dhana inayoweza kututofautishia kati ya utendi simulizi na utendi andishi ambapo;

Utendi simulizi huwasilishwa kwa njia ya   kunenwa au kuimbwa na ala za muziki. Tendi nyingi za Kiafrika hutumia mbinu mbalimbali katika uwasilishaji wake miongoni mwa njia hizo ambapo utendi huweza kusimuliwa ni pamoja na  njia ya ushairi au nudhumu yaani kuimbwa. Mfano , Katita utendi wa Sara wa jamii ya Manika  ameonyesha wimbo aliouimba Sara pamoja na Kaka yake Yamuri Jabate, ambapo unajitokeza urudiaji rudiaji wa chorus. Mfano;

  5. Chorus : Ah! Sara is sung for those of one voice.

                        Dońt you see it?

                        Sira Mori: Sara!  sara is sung for those with promises.

                        Dońt you see it?

Wakati utendi andishi utendaji au uwasilishaji wake hufanyika kwa njia ya usomaji (kusomwa) bila kuwepo kwa ala za muziki  ambapo mtu yeyote anayejua kusoma  na kuandika huwa na ruhusa ya kusoma  kitabu ama kazi hiyo. Mfano utendi wa Fumo Liyongo .

Wahusika: Ni watu, wanyama au vitu vitumikavyo katika kazi ya kisanaa ya kifasihi, ( Msokile 1999:32). Vile vile  dhana ya wahusika ndiyo hutuwezesha kutambua utofauti uliopo kati ya utendi simulizi na utendi andishi ambapo:

Utendi simulizi,  hutumia wahusika changamano ( wanyama, watu, mazimwi, miungu). Mfano katika Utendi wa Rasi ÌGhuli  msimulizi ametumia wahusika mbali mbali walio binadamu na wasio binadamu ambao ndio wameijenga na  kuikamilisha hadithi nzima. Wahusika hao ni kama vile ;  wahusika binadamu ambao wanaongozwa na Mtume Muhamadi na Masahaba wa wafuasi wa Kiislamu. Pia kuna binadamu Makafiri wanaoongozwa na Rasi 'lGhuli. Vile vile wahusika wasio binadamu ni kama vile Malaika, miungu na Ibilisi  ambako wahusika hawa wamejitokeza katika Uk 13-19 katika ubeti wa 350-362.

mfano: ubeti wa 354.

“Kiswahili jiburili                                                   359. Akusalamu jalali

      Kanituma nikujiye                                                     Tuma mtu amwendee

     Akamwambia Rasuli                                                 Salamu nyingi kathiri

Na maneno nikwambiye.                                          Sultani wa kufari

ubeti wa 473." Ibilisi maluuni                                          475. Akangia sanamuni

   Sikuzaa sikuzawa                                                        Naumba nikiumbua

  Achondoka iyo hini                                                       Sultani kumghuni

 Naua na kufufua                                                            Ndimi wahidi Quhari

Wakati, utendi andishi hutumia wahusika wanadamu  kuiumba kazi hiyo ya utendi andishi ili iweze kufikisha ujumbe wake kwa hadhira ama jamii iliyokusudiwa. Mfano katika Utendi wa Fumo Liyongo mwamdishi ametumia wahusika binadamu wengi miongoni mwao ni pamoja na ; Sultani Daudi Mringwari ambaye aliyepanga kumuua Liyongo, Kijakazi Saada aliyekua anampelekea Liyongo chakula gerezani pia muhusika  Liyongo ambaye ndiye mhusika mkuu na mwanaume mwenye nguvu ya uganga au sihiri. Hilo linajidhihirisha katika muujiza wa nguvu zake  zilizokuwa  katika  kitovu chake, ambapo hapakuwa na kitu cha kumdhuru ila kudungwa sindano ya shaba kitovuni. Yamejitokeza  shairi la Fumo Liyongo ubeti wa 143-144;

143. " Nisikiya wangu baba                                                      144. "Jamii silaha piya

 Liniuwalo ni haba                                                                      Haziniuwi swabiya

 Ni msumari wa shaba                                                               Ila nimezokwambiya

    Kitovuni nikitiya.                                                                       Ni ya kweli yote piya.

Uhifadhi: Ni kitendo cha kutunza kazi za kisanaa za kifasihi ili zidumu kwa mdaa mrefu na ziweze kutumiwa na vizazi vingine. Hivyo basi uhifadhi ni dhana inayotutofautishia kati ya utendi simulizi na utendi andishi ambapo;

 Utendi simulizi huhifadhiwa kichwani. Kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo wakati wowote, mahali popote na bila gharama yeyote. Kazi ya utendi  iliyohifadhiwa kichwani ni hai kwasababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Pia kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, na hata miondoko ambapo mbinu hizo  huifanya kazi  yake ipate uhalisia zaidi mbele ya hadhira. Mfano katika Utendi wa Fumo Liyongo msanii ameonyesha mbinu hizo kama vile "kucheza" ambapo watu walikusanyika kucheza ngoma ya Gungu iliyopigwa kwa lengo la kumkamata Liyongo ili wamuue , vile vile walicheza pale Liyongo alipoambiwa aombe ombi la mwisho ili auawe naye akaomba apigiwe ngoma ya Mwao na Gungu ili wacheze wote. Haya yanajitokeza katika ubeti wa 80_81 pamoja  na ubeti wa 112 na 117.

    80. Sulutwani kabaini                                               81. "Kwa wanaume na wake

          Ma-Shaha walo muini                                                na Liyongo, mumwalike

          kawambiya kwa sirini                                                 naazimu nimshike

         "Pijana," gungu hwambiya                                        ni siri nimewambiya.

112.Na ngoma na nyingi kusi                                      117. Wakiinuka kuteza

           kusisalie unasi                                                               Liyongo akatokeza

       ikawa kama harusi                                                        khaufu zaliwakaza

      watu wakiangaliya.                                                         mbio zikawapoteya.

 

 Wakati utendi andishi huhifadhiwa kwenye maandishi ( Vitabuni)ambapo kazi ya msanii huwa katika makala ama kitabu maalumu na kazi hii haipotezi fani  na maudhu yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha. Mfano utendi wa Mwanakupona ambao unatoa mawaidha kwa msichana kuhusu unyumba na maisha kwa ujumla katika  jamii ya waswahili wa tabaka la juu. Hivyo mbali na Mwanakupona Binti Mshamu  kuuandika utendi huu kwa mwanae Mwana Hashimu Binti Mataka kwa  lengo la kumpa wosia kuhusu kumheshimu mmewe katika ndoa ambapo alimwita mjinga katika ubeti wa 92

        92 . Na sababu ya kutunga

                Si shairi ni malenga

                 Nina kijana muinga

                 Napenda kumuusia.

 Vilevile aliandika kwa kuwataka vijana wengine wa kike wausome pia ili wawatii waume wao katika ubeti wa 94 _95. Ambapo pia wanawake wengine wa Kenya waliupenda wosia huo na wakaufanyia kazi na hata leo wanaendelea kufunzwa pale  wanaposoma utendi huo.

 

 

              94. Someni nyute huramu                           95. Somani mite ya nganu

                    maana muyafahamu                                   mutii waume zenu

                    musitukue laumu                                               musipatwe na zitunu

                mbee za mola Jalia                                             za akhera na dunia.

 

Mazingira (mandhari) na wakati: Wamitila (2002), " Mandhari ni ile arki au elementi ambayo hutufichilia wapi na lini matukio yalifanyika . Anaongezea kusema kuwa, neno hili hutufichilia wakati na sehemu matukio yalipotokea . Nafasi ya mandhari katika utendi huwa ni uendelezwaji wa maudhui ya utungo. Hivyo basi mandhari na wakati hututofautishia kati ya utendi simulizi na andishi ambapo;

Utendi simulizi hubadilika kulingana na wakati na mazingira. Hii ni kwasababu hadithi iliyosimuliwa mwaka jana haiweze kufanan na itakayosimuliwa mwaka huu kwani baadhi ya vitu hutoweka katika mazingila na vingine huongezeka.  Pia matukio katika utendi simulizi huhadithiwa kwa kutaja mazingira halisi na penginepo mhusika husimulia tukio hilo akiwa katika sehemu ile inayozungumziwa. Mfano katika utendi wa Fumo Liyongo  msanii ametuonyesha mazingira yaliyotumika wakati wa matukio maalumu kama vile ; Gerezani_ mahali ambapo Sultani Daudi Mringwari aliamuru Liyongo  atiwe ili aje auwawe kwa kuhofia kuwa atamnyang'anya madaraka kutokana na ushujaa aliokuwa nao Liyongo, mazingira mengine ni Kisimani_ mahali ambapo Liyongo  alipiga goti na kutia mshale katika upinde huku kauelekeza mjini na kukata roho , hii ilitokea mara baada ya mtoto wake kutumwa na Sultani akamwue kwa kumchoma sindano ya shaba (Ubeti wa 181_182).

             181. " Akapija ondo lake                                                     182. Na hapo nami t'asema       

                     katambika chembe chake                                                   ni karibu ya kisima

                    kama hai ada yake                                                                  watu hawakusimama

                   chembe utani katiya.                                                                kwa wut'e walikimbiya.

 Wakati, utendi andishi haubadiliki kulingana na wakati na mazingira kutokana na kuwa katika kitabu au makala maalumu hivyo ni vigumu kabadilika mahali popote pale watakapo usoma watasoma yale yale yaliyomo kitabuni na katika wakati wowote ule labda hadi pale mwandishi atakapoamua kubadilisha mwenyewe na kuandika upya ile sehemu aliyotaka kufanya marekebisho . Mfano katika utendi wa Mwana Kupona Binti  Mshamu Nabhnany  ambapo inasemekana aliutunga utenzi huo akiwa mgonjwa (inasemekana aliugua maradhi ya tumbo la uzazi). Alihisi kuwa asingepona , hivyo akaamua kutunga utenzi ili uwe ni wosia kwa binti yake ambaye angebaki bila ya uongozi wa mama( Ubeti wa 2 na 90_91). Hivyo basi utenzi huo haujabafilika bado unasomwa hivo na watu mbali na kwamba wengine hauwahusu ( wazazi wao sio wagonjwa).

 

            2. Maradhi yamenishika

              hatta yametimua mwaka

                sikupata kutamka

                neno lema kukwambia.

          90. Ntungile utungo hunu                                  91. Ntungile nili saqimu

                 kwa zehemu na zitunu                                       moyo usina fahamu

               kwa qadha yako Dayyanu                                     usomeni Islamu

                na hukumuzo Jalia.                                             mkiongozana ndia

 Hitimisho: Pamoja na  kuwepo kwa tofauti kati ya tendi hizi mbili ( utendi simulizi na utendi andishi) ,  tendi hizi ni muhimu kwa jamii kwan hutuwezesha kujua mambo mbali mbali kutokana na majukumu yake kama vile ;  kutoa wasifu wa shujaa mfano Shujaa Liyongo, kukuza uzalendo kwa kuhimiza wengine kutoogopa kwa kuwaiga mashujaa, pia kukuza vipaji vya utunzi wa kazi hizi hususani  kwa wanawake kwa kuiga mfano wa Mwanakupona Binti Mshamu.

 

 

 

 

 

MAREJEO.

Mulokozi, M.M.(1996). Fasihi ya kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania : Dar es salaam.

Mulokozi, M.M.(Mh) (1999). Tenzi Tatu za kale. TUKI: Dar es salaamu.

Msokile.(1999): Tafsiri ya dhana ya wahusika katika kazi ya kifasihi ya kisanaa.

Wamitila .(2002): Tafsiri ya dhana ya mandhari/mazingira na wakati katika kazi ya kifasihi   ya

kisanaa.

Wamitila. (2003): Tafsiri ya dhana ya utendi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

International Law

KATIBA YA KIKUNDI